Sunday, September 25, 2016

Dangote Bilionea anayenyimwa haki ya kuinunua Arsenal

MFANYABIASHARA maarufu nchini Nigeria, Aliko Dangote, anatajwa kuwa mbioni kuinunua klabu ya Arsenal. Dangote anataka kuhakikisha Arsenal inakuwa yake katika kipindi kisichozidi miaka minne kwa sasa. Kwa mara ya kwanza, taarifa za tajiri huyo kuitaka Arsenal zilianza kuvuma mwaka uliopita, lakini sasa ameonekana kuwa ‘siriazi’ kidogo. Imeripotiwa kuwa Dangote ameufufua mpango huo baada ya Arsenal kuisambaratisha Hull City mabao 4-1 ambapo Alexis Sanchez alipasia nyavu mara mbili. “Labda miaka mitatu mpaka minne. Tatizo ni kwamba bado kuna changamoto nyingi. Natakiwa kuzimaliza na ndipo kuanza mchakato huo. Hapo ndipo nitakapoweza kushughulikia hilo,” alisema Dangote. Kwa sasa, Mmarekani Stan Kroenke ndiye mwenye hisa nyingi katika klabu ya Arsenal, akiwa na asilimia 67. Ana mpunga mrefu Kwa mujibu wa taarifa, Dangote anatajwa kuwa na utajiri wa pauni bilioni 8.3. Mshua huyo ndiye anayeongoza kwa utajiri barani Afrika, kwa mujibu wa Jarida maarufu la Marekani la Forbes. Miaka miwili iliyopita, Dangote alishika nafasi ya 67 kwenye orodha ya watu matajiri duniani, alipombwaga bilionea wa Kiarabu, Mohammed Hussein Al Amoudi na kuwa Mwafrika mwenye fedha nyingi duniani. Mashabiki watafurahi kinoma Huenda Dangote akapata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Arsenal ambao wameonesha kutokuwa na imani na Kroenke. Kroenke amekuwa akikosolewa vikali na mashabiki wa klabu hiyo kutokana na ‘ubahili’ wake kwenye soko la usajili. Aahidi neema Emirates Dangote amesema amekuwa na mafanikio makubwa katika biashara zake, hivyo ana uwezo wa kumiliki timu yenye mafanikio pia. “Siyo kununua Arsenal na kuona mambo yakiendelea kwenda kiholela. “Kwa sasa, kwa kile tunachokabiliana nacho, tuna miradi ya zaidi ya Dola bilioni 20, siwezi kufanya vyote kwa pamoja.” Aidha, Dangote aliongeza kuwa anaamini Arsenal inahitaji aina tofauti ya umiliki ili kuleta ushindani kwenye mbio za kuwania taji la Ligi Kuu England. “Wanafanya vizuri, lakini wanahitaji mwelekeo mpya wa kimkakati. Wanahitaji mwelekeo mwingine kuliko walionao hivi sasa, ambao ni wa kukuza wachezaji na kuwauza,” alisema bosi huyo. Ni mtoto wa kishua Ule usemi wa Waswahili kuwa maji hufuata mkondo unadhihirika wazi kwa Dangote. Bosi huyo alizaliwa mwaka 1957 katika Jimbo la Kano. Ni mjukuu wa Alhaji Alhassan Dantata, aliyekuwa mfanyabiashara tajiri na maarufu nchini Nigeria kabla ya kufariki mwaka 1955. Kumbe simenti ni bonge la dili! Kama ulikuwa hujui, kipato kikubwa cha Dangote kinatokana na kampuni yake iliyopo jijini Lagos ambayo inashughulika na uzalishaji wa simenti. Mbali na Nigeria, kampuni yake hiyo ina matawi katika nchi za Cameroon, Ethiopia, Zambia na Tanzania. Inazalisha tani milioni 30 kwa mwaka na Dangote ameeleza mpango wake wa kuongeza zaidi ifikapo mwaka 2018. Ameyumba kiuchumi Hivi karibuni, thamani ya fedha ya Nigeria (Naira) iliporomoka na hilo lilisababisha Dangote kupoteza pauni bilioni 3.3. Ana mishe kibao Ukiachana na simenti, kampuni yake ya Dangote Group inajihusisha na uzalishaji wa chumvi, sukari na ngano. Pia, amefanya uwekezaji mkubwa kwenye uchimbaji wa mafuta na nishati ya gesi, huku biashara zake hizo zikisambaa katika nchi 15. Ni shabiki wa Arsenal Mwaka uliopita, Dangote aliweka wazi mapenzi yake kwa Arsenal. Alisema anataka kununua klabu hiyo kwa sababu amekuwa akiishabikia kwa kipindi chote cha maisha yake. Hata yeye hamkubali Wenger Kwa upande mwingine, inaonesha wazi kuwa Dangote si mpenzi wa kocha wa sasa wa Arsenal, Arsene Wenger. Tajiri huyo aliwahi kusema kuwa angemfukuza kazi Mfaransa huyo ikiwa angeinunua Arsenal kwa kipindi chote cha mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

bab