Sunday, October 9, 2016
Hata Baada ya Kudai Kuzifanyia Marekebisho Simu nyengine ya Galaxy Note 7 yashika moto US
Simu ya pili ya Samsung Galaxy Note 7 iliodaiwa kuwa salama na kampuni hiyo imeshika moto nchini Marekani,kulingana na vyombo vya habari.
Samsung ililazimika kutoa simu nyengine mpya ya simu hiyo aina ya smartphone kufuatia malalamishi ya betri zinazolipuka.
Mtu mmoja mjini Kentucky alisema kuwa alishtuka baada ya kuamka na kupata nyumba yake imejaa moshi ,kulingana na vyombo vya habari nchini humo.
Hatua hiyo inajiri baada ya simu nyengine aina ya Note 7 iliokuwa imerekebishwa kushika moto ndani ya ndege ya SouthWest Airlines siku ya Jumatano.
''Simu hiyo ni miongoni mwa zile zilizorekebishwa, kwa hivyo nilidhani ziko salama'',alisema Michael Klering wa Nicholasville,Kentucky.
Aliongezea kwamba simu hiyo haikuwa imewekwa katika chaji wakati iliposhika moto katika nyumba yake siku ya Jumanne.
Mtandao wa Wikileaks wafichua hotuba ya Clinton
Mtandao wa Wikileaks, umechapisha kile unachosema kuwa hotuba ya kibinafsi ya Bi Hillary Clinton, kwa wakuu na wanaharakati.
Katika mojawapo ya hotuba, ameziambia benki nchini Marekani kuwa ziko katika nafasi nzuri mno ya kuleta mabadiliko katika sekta ya kifedha, huku katika hotuba nyengine akisema kuwa anaunga mkono biashara huru ya wazi ndani na nje ya nchi.
Bi Clinton amekataa kuchapisha hotuba hizo, iliyompa mamilioni ya dola kabla ya kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.
Mpinzani wake katika chama cha Democrat wakati huo Bernie Sanders alikuwa amemtaka kutoa nakala za hotuba hiyo ,ambazo zinadaiwa kumpatia dola milioni 26.
Ufichuzi huo wa Wikileaks huenda ukatawala habari wikendi hii huku wachanganuzi na wanasiasa wakibashiri kwamba hatua hiyo itawapendelea waliokuwa wagombea Marco Rubio,Jeb Bush na hata Ted Cruz.
Nyota Muislamu azuiwa kuigiza mchezo wa Kihindu India
Wahindi wa mrengo wa kulia wamemlazimisha nyota wa filamu za Bollywood Nawazuddin Siddiqui kutoshiriki katika hafla ya sherehe ya Kihindu,''kwa sababu ni Muislamu''.
Baadhi ya wanachama wa shirika la Kihindi la Shiv Sena walisema kuwa wanapinga muigizaji Muislamu mbele ya jukwaa huko Ramlila,ambapo sherehe za uigizaji zinazohusiana na dini ya Hindu Ramayana hufanyika mbali na taifa lote la India.
Nyota huyo alisema kuwa kushiriki katika sherehe hiyo ilikuwa ndoto yake tangu akiwa mdogo.
Shirika la Shiv Sena hutumia ghasia na vitisho ili kusukuma wazo ama ajenda yake.
Katika sherehe hiyo Wahindi husherehekea zuri dhidi ya ovu kufuatia ushindi wa mungu wa kihindi Ram dhidi ya shetani wa kifalme mwenye vichwa 10 Ravana .
Vijiji nchini India hufanya uigizaji huo na hutumia muda mwingi kujiandaa.
Miaka 115 ndio 'mwisho wa maisha' kwa binadamu
Wanasayansi nchini Marekani wamesema baada ya kufanya utafiti wamegundua huenda umri mkubwa zaidi ambao binadamu anaweza kuishi duniani ni miaka 115.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la Nature.
Wamefikia uamuzi huo baada ya kutathmini data zilizokusanywa kwa miaka mingi kuhusu maisha ya mwanadamu.
Wanasema kunao watu wanaoweza kubahatika waishi miaka kadha zaidi ya 115 lakini utakaa sana kabla ya kupata mtu hata mmoja aliyefikisha umri wa miaka 125.
Wanasema utahitaji "kutafuta katika sayari 10,000 za dunia" kupata angalau binadamu aliyeishi miaka 125.
Aliyedanganya kuwa ni mzee akamatwa Marekani
Mzee mwenye watoto 70 na wajukuu 300 Tanzania
Lakini baadhi ya wanasayansi wamekosoa utafiti huo, na baadhi hata wakautaja kama dhihaka.
Umri wa binadamu kuishi umekuwa ukiongezeka tangu kuanza kwa karne ya kumi na tisa kutokana na kugunduliwa kwa chanjo, wanawake kujifungua kwa njia salama zaidi na juhudi za kukabiliana na maradhi kama vile saratani na maradhi ya moyo.
Lakini umri unaweza kuendelea kuongezeka?
Kundi hilo la watafiti kutoka New York lilichunguza data kutoka kwa Hazina Data ya Vifo vya Binadamu na vifo vya watu waliozidi umri wa miaka 110 Japan, Ufaransa, Uingereza na Marekani.
Wanasema uchunguzi wao ulibaini ongezeko la umri wa kuishi miongoni mwa wale wazee kabisa ni kama umefikia upeo.
Prof Jan Vijg, mmoja wa watafiti anayetoka Chuo Kikuu cha Matibabu cha Albert Einstein, aliambia BBC News: "Miongoni mwa watu wa umri wa miaka 105 na zaidi, hakujakuwa na mabadiliko makubwa, na hili linakuonyesha kwamba tunafikia upeo wa maisha ya binadamu.
"Kwa mara ya kwanza katika historia, tumeweza kuona hili, upeo huu, ambao ni miaka 115."
Mtu aliyeishi miaka mingi zaidi
eanne Calment ndiye binadamu ambaye anatambuliwa kuwa aliyeishi miaka mingi duniani na ambaye kuna stakabadhi rasmi za kuthibitisha hilo.
Alikuwa na miaka 122 alipofariki 1997.
Tangu wakati huo, hakuna aliyekaribia umri huo.
Dhihaka?
Prof James Vaupel, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti kuhusu watu ya Max Planck ni mmoja wa wanaopinga utafiti huo.
Anasema zamani, wanasayansi walikuwa wamedai umri wa juu zaidi anaoweza kuishi binadamu ni miaka 65, wakaenda kwa 85 na baadaye wakasema miaka 105 lakini historia ilidhihirisha baadaye kwamba walikuwa wamekosea.
"[Utafiti huu] hauongezi ujuzi wowote kuhusu tutaishi kwa muda gani."
Mwanamke avunja rekodi ya ndevu
Wanasayansi waunda ngozi kuziba uzee
Utafiti, ambao umeangazia wanyama, hata hivyo umedokeza huenda kukawa na upeo kwa maisha ya viumbe.
Prof Jay Olshansky, wa Chuo Kikuu cha Illinois, anasema panya huishi siku 1,000, na mbwa siku 5,000 hivi na "binadamu huenda wanakaribia upeo wa uwezo wao wa kuishi".
Kuzuia uzee?
Changamoto kuu ni kwamba binadamu hajaweza kupata mbinu ya kuendelea kuishi baada ya kuzeeka sana.
Hili sana huamuliwa na maelezo kwenye chembenasaba au DNA.
Kwa hivyo, juhudi zozote za kuongeza umri wa binadamu kuishi zitahitaji kufanya jambo la ziada na si tu kutibu magonjwa.
Mzee wa umri wa miaka 145 Indonesia
Juhudi hizo zitahitajika kupata njia ya kuzuia kuzeeka kwa kila seli ndani ya mwili.
Prof Jan Vijg ameongeza: "Ili kuwezesha watu kuishi miaka 120, 125 au 130 labda, tutahitaji kufanya ugunduzi mkubwa."
Viongozi wa Republican wazidi "kumtema" Donald Trump
Viongozi wakuu wa chama cha Republican wanazidi kuondoa uungaji wao mkono kwa Donald Trump kwa matamshi yake ya kuwadhalilisha wanawake.
Miongoni mwa wanasiasa wa hivi punde zaidi ni pamoja na aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani Condoleezza Rice, na aliyegombea kiti cha urais nchini humo, Senator John McCain.
Lakini Trump amesema kwamba hatajiondoa kutoka katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti hicho licha ya malalamishi kutoka kote duniani kutokana na matamshi yake ya kuudhi kuwahusu wanawake, aliyo-yatoa mwaka 2005.
Zaidi ya wanasiasa 24 wa chama chake cha Republican, sasa wamesema hadharani kuwa hawamuungi mkono bilionea huyo na wanamtaka kumuachia mgombea mwenza Mike Pence nafasi ya kuwania kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu wa Marekani hapo mwezi Ujao.
Miongoni mwa wanaolaani matamshi hayo ya Trump ni pamoja na mkewe Trump- Melania.
Amesema kuwa licha ya kuendelea kumuunga, analaani matamshi hayo mapotovu dhidi ya wanawake.
Spika wa Bunge Paul Ryan, alizomewa na kushangiliwa kwa wakati mmoja, katika mkutano mmoja wa kisaiasa baada ya kukataa kutumia jukwaa moja na Bwana Trump.
Subscribe to:
Posts (Atom)