Sunday, September 25, 2016
Aliyemtembeza Lowassa afariki ghafla
AHMED Mussa Mseha, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kata ya Hamgembe, Manispaa ya Bukoba amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka ghafla akiwa kwenye ofisi ya wilaya ya chama hicho, anaandika Mwandishi Wetu.
Kifo hicho kimetokea jana mchana baada ya katibu huyo kumaliza ziara ya Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani mkoani Kagera alipokwenda kuwafariji waathirika wa tetemeko la ardhi.
Eustace Mbalilaki, Katibu Mwenezi wa Chadema Bukoba mjini amesema, katibu huyo baada ya kumaliza ziara ya Lowassa, alikwenda katika shughuli zake za kawaida, ndipo akiwa huko alianguka ghafla na kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kagera.
“Katibu tulimuacha katika kata yake baada ya kumaliza ziara ya Lowassa, ndipo mchana tukapata taarifa kwamba amefariki dunia baada ya kuanguka.
“Kama binadamu huwezi kushangaa kufikwa na umauti ingawa ni masikitiko kwani hatujui siku wala saa ya kufa kwetu maana Katibu huyo, hakuwa mgonjwa,” amesema.
Juma Nyakina, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Kagera amesema, kifo cha katibu huyo kimetokana na mshtuko wa moyo.
Lowassa alikwenda mkoani Kagera kuwafariji waathirika wa tetemeko la ardhi ambapo Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya maelfu ya wananchi waliofika katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba, kumlaki.
Lowasa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema aliwasili Bukoba jana saa 5:30 asubuhi kwa ajili ya kuwapa pole waathirika wa tetemeko hilo lililotokea tarehe 10 Septemba mwaka huu ambapo watu 17 walifariki dunia.
Idadi kubwa ya watu walifika katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba mapema asubuhi, huku kukiwa na umati mkubwa wa vijana waendesha bodaboda ambao walijaa nje ya uwanja huo.
Kutokana na idadi ya watu inazidi kuongezeka, Jeshi la Polisi mkoani humo lililazimika kupeleka askari wake wenye silaha kulinda usalama na kuufuatilia hatua kwa hatua msafara wa Lowassa.
Baada ya Lowassa kuwasili na wananchi kuanza kushangilia, polisi walirusha mabomu kadhaa ya machozi kuwatanya wananchi hao ambao baadhi walikuwa kwenye sare za Chadema.
Pamoja na wananchi hao kusambaratishwa kwa mabomu ya machozi, walibaki mafungu mafungu katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Bukoba na baadhi yao kuamua kuufuata msafara Lowassa uliokuwa ukielekea maeneo ya waathirika Mtaa wa Omukishenye, Kata ya Hamgembe ambapo aliwapa pole wakazi wa mtaa huo kwa niaba ya wakazi wa kata nzima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
bab